Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Visa vipya vya Ebola vyathibitishwa Guinea WHO yaonya uwezekano wa mlipuko zaidi

Visa vipya vya Ebola vyathibitishwa Guinea WHO yaonya uwezekano wa mlipuko zaidi

Shirika la afya duniani WHO limepeleka timu ya wataalamu  Kusini mwa mkoa wa  Nzérékoré  nchini Guinea baada ya visa vipya viwili vya Ebola kubainika na kuthibitishwa  katika maeneo ya kijijini. John Kibego na maelezo zaidi

(TAARIFA YA KIBEGO)

Maafisa wa afya wa Guinea walitoa taarifa kwa WHO na wadau wake Machi 16  kwamba kuna vifo vitatu  vinavyotatanisha  katika wiki za karibuni kwenye kijiji cha Koropara  na watu wengine wa familia hizo hivi sasa wana dalili zinazofanana na Ebola.

Wizara ya afya ya Guinea, WHO, kitengo cha Marekani cha kudhibiti magonjwa CDC na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani UNICEF, wamepeleka wachunguzi Machi 17, na vipimo vikachukuliwa kutoka kwa watu wanne, na mama na mwanae wa miaka mitano ambao ni ndugu wa mmoja wa waliokufa wamethibitishwa kuwa na virusi vya Ebola na wamepelekwa kwenye kituo cha tiba.

Visa hivyo vipya vimethibitishwa siku ambayo WHO imetangaza kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa huo katika nchi jirani ya Sierra Leone. Shirika hilo linaonya kwamba kulipuka upya kwa ugonjwa huo kutarajiwe, na nchi tatu zilizoathirika awali an kwamba ziwe makini na uwezo wa kuzuia, kubaini na kukabiliana na mlipuko.