Imax na UNEP zazindua mkakati wa "Big Picture" kuchagiza utunzaji mazingira

Imax na UNEP zazindua mkakati wa "Big Picture" kuchagiza utunzaji mazingira

Kampuni ya filamu ya Imax, kwa kushirikiana na Shirika la Mpango wa Mazingira (UNEP), imezindua leo mkakati kabambe wa “Big Picture”, kupigia chepuo utunzaji wa mazingira.

Taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti ya UNEP imesema mkakati huo ni sehemu ya dhamira ya kampuni ya Imax kuelimisha, kuburudisha na kuhamasisha watazamaji wake kote duniani, kwa kuelewa kuwa hatua vitendo wanavyofanya watu katika maisha yao kila siku vinaweza kuathiri pakubwa mustakhbali wao na sayari dunia.

Chini ya mkakati huo, Imax inalenga kushirikiana na UNEP kushughulikia masuala kadhaa ya kimazingira, kijamii na kiuchumi yanayoikabili dunia sasa.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNEP, Achim Steiner amesema amekuwa na haya ya kusema kuhusu mkakati huo..

“Sehemu ya ubia wetu itahusu kuunga mkono ushiriki wa vijana, kupitia mashindano ya filamu fupi, ambayo yatawatia moyo vijana waunda filamu kusimulia hadithi za malengo ya maendeleo endelevu. Pia kutakuwa na makala ya elimu kuhusu masuala muhimu ya mazingira na malengo ya maendeleo endelevu. Ikiwa hadithi ya 2015 ilikuwa dhamira ya kisiasa, natumai kuwa hadithi ya 2016 kwenda mbele itakuwa kuhusu wote kuchukua hatua. Ubia huu kati ya UNEP na Imax utakuwa adhimu katika kuwezesha hayo kufanyika.”