Hatua kidogo sana zimepigwa kukabiliana na ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni:UM
Katika kuelekea siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi wa rangi hapo Jumatatu Machi 21, dunia inashuhudia ongezeko la kutisha la chuki na hotuba za chuki dhidi ya wageni , wamesema wataalamu watatu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ubaguzi na ubaguzi wa rangi.
Kwa mujibu wa wataalamu hao Mutuma Rutereere mwakilishi maalumu kuhusu mifumo ya kisasa ya ubaguzi wa rangi, mwakilishi maalumu na mwenyekiti wa kundi maalumu la waatalamu kuhusu watu wenye asili ya Afrika, Mireille Fanon Mendes-France na mwenyekiti wa kamati ya utokomezaji wa ubaguzi wa rangi Jose Francisco Cali Tzay, juhudi zaidi zinahitajika kufanywa na serikali kote duniani kulinda makundi yaliyo katika hatari na kuwaadhibu wanaotekeleza ukatili huo.
Wameongeza kuwa miaka 15 baada ya mkutano wa Durban hatua ndogo sana imepigwa kukabiliana na ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya Uafrika, ubaguzi kwa misingi ya rangi, chuki dhidi ya wageni na masuala mengine yanayoshabihiyana na hayo na badala yake kunashuhudiwa ongezeko kubwa la chuki, na hotuba za chuki dhidi ya wageni duniani kote.
