Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua za haraka za Sierra Leone zimemaliza hofu ya mlipuko wa Ebola:WHO

Hatua za haraka za Sierra Leone zimemaliza hofu ya mlipuko wa Ebola:WHO

Shirika la afya duniani, WHO limethibitisha kumalizika kwa hofu ya mlipuko mpya wa Ebola nchini Sierra Leone. Tangazo hilo limekuja siku 42 tangu kuthibitishwa kwa mgonjwa ambaye alipimwa mara mbili na kubainika hana tena virusi vya ugonjwa huo. Assumpta Massoi na taarifa kamili.

(TRAARIFA YA ASSUMPTA)

Kwa mujibu wa WHO huu ni wakati muhimu sana kwa taifa hilo na hasa kwa mzunguko wa virusi vya Ebola ambao unatarajiwa kuisha bila mtu yoyote kuambukizwa ili kutangazwa kutokomeza kabisa ugonjwa huo.

Hata hivyo baada ya kutangaza hofu ya mlipuko imekwisha WHO imesema ni hatua nyingine kubwa kwa Sierra Leone.

Mafanikio ya kupambana na ugonjwa huo ni kutokana na hatua za haraka za serikali, washirika wake na watu kwa ujumla. Shirika hilo limeongeza kwamba udhibiti wa haraka wa ugonjwa huo

unaonyesha kwamba ni jinsi gani maandalizi ni muhimu katika kukabiliana na dharura ya magonjwa katika ngazi ya kitaifa, kiwilaya na kijamii. Hata hivyo shirika hilo limeonya kwamba Sierra Leone na nchi zilizoathirika awali za Liberia na Guinea bado ziko katika hatari ya mlipuko mwingine na hivyo nchi zote tatu lazima ziwe katika tahadhari na kuwa tayari kukabili mlipuko kama utatokea.

Ebola imekatili maisha ya watu zaidi ya 11,300 na kuathiri familia na jamii katika ngazi mbalimbali.