Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wadau wa misaada ya kibinadamu wahaha kuwafikia maelfu Ramadi

Wadau wa misaada ya kibinadamu wahaha kuwafikia maelfu Ramadi

Wadau wa misaada ya kibinadamu wanahaha kutoa msaada wa dharura kwa takribani watu 35,000 ambao wametawanywa na machafuko mapya kwenye maeneo yasio fikika ya Ramadi Magharibi.

Lise Grande mratibu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu amesema maelfu ya watu ambao wamekwama mjini Heet kwa miezi kadhaa wanajaribu kukimbilia kwenye usalama. Umoja wa Mataifa hauna fursa ya kutosha kuwafikia na unahofia kwamba baadhi ya familia ambazo zinajaribu kutoroka wako karibu na eneo la mapigano na kuweka usalama wao hatarini.

Familia hizo zilizotawanywa na machafuko zinapokea chakula ambacho kipo tayari kuliwa, maji safi ya kunywa na vifaa vya usafi kwa kupitia mpango maalumu unaosimamiwa na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa(UNICEF) na lile la mpango wa chakula duniani(WFP). Mpango huo unafadhiliwa na Shirika la Idadi ya Watu Duniani(UNFPA), Shirika la Kimataifa la Uhamiaji(IOM) na mashirika mengine tisa yasiyo ya kiserikali.

Huduma za afya zinazotolewa na WHO ambalo limetuma magari mawili yanayotumika, kama vituo vya afya na wataalamu wa afya wawili. Kabla ya watu kutawanywa Heet, watu wengine 53,000 walikimbia machafuko katika jimbo la Anbar mwanzoni mwa mwaka.