Skip to main content

Waziri Mkuu wa Canada achukua hatua kwa ajili ya usawa wa kijinsia

Waziri Mkuu wa Canada achukua hatua kwa ajili ya usawa wa kijinsia

Waziri Mkuu wa Canada Justin Trudeau amezungumzia hatua zilizochukuliwa kwenye nchi yake ili kufikia usawa wa kijinsia, akisema bado safari ni ndefu, hasa kwa upande wa ukatili wa kingono dhidi ya wanawake kutoka jamii za watu wa asili.

Amesema hayo akihudhuria mjadala maalum ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusiana na masuala ya wanawake UN women leo mjini New York, kando ya mkutano wa 60 wa Kamesheni ya Hali ya Wanawake CSW.

Ameeleza sababu ya kuwa mtetezi wa haki za wanawake.

(Sauti ya Bwana Trudeau)

“Kwanza, nitaendelea kusema kwa sauti kubwa mimi ni mtetezi wa wanawake, mpaka watu hawatajali. Haipaswi kushtua watu. Na kwa sababu bado inashtua watu, basi inamaanisha kwamba bado tunapaswa kuendelea kutumia neno hilo.”

Miongoni mwa mafanikio yaliyopatikana Bwana Trudeau ametaja usawa wa mishahara, na uteuzi wa baraza la mawaziri lenye asilimia 50 ya wanawake, akiongeza kwamba lengo lake ni kuwezesha wanawake zaidi kushirikiana katika masuala ya kisiasa, hasa bungeni ambapo hadi sasa nchini Canada wanawake wako asilimia 26 tu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa UN Women Phumzile Mlambo Ngcuka amesema sheria ni mbinu muhimu katika kuendeleza usawa wa kijinsia. Ameongeza kwamba lazima wanaume, viongozi wa dini, na vyombo vya habari vishirikishwe katika jitihada hizo.

Hatimaye Bi Mlambo Ngcuka amesema usawa wa kijinsia haupaswi kuwa lengo la muda mrefu, bali unapaswa kutimizwa ifikapo mwaka 2030.