Skip to main content

Baadhi ya nchi za Ulaya hazizingatii kabisa haki za binadamu- Mtaalam wa UM

Baadhi ya nchi za Ulaya hazizingatii kabisa haki za binadamu- Mtaalam wa UM

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu za wahamiaji, François Crépeau, amesema Ulaya haiwezi kupuuza wajibu wake kwa wahamiaji na kuisukumia Uturuki jukumu hilo.

Bwana Crépeau amesema hayo kabla ya kuanza mkutano wa Muungano wa Ulaya wa tarehe 17-18, ambapo viongozi wa jumuiya hiyo ya nchi 28 watajadili kuhusu makubaliano mapya na Uturuki kuwarejesha wahamiaji wote wanaovuka mpaka kuingia Ugiriki kwa njia isiyo halali, wakiwemo wakimbizi.

Amesema zamani nchi za Ulaya ziliwajibika kwa kutunga sheria kuhusu haki za binadamu na ulinzi wa kibinadamu, lakini sasa zinataka kuyatelekeza majukumu yao kwa manufaa ya kisiasa na kuisukumia Uturuki wajibu wao wakati huu wa mzozo mkubwa zaidi wa uhamiaji tangu vita vikuu vya pili vya dunia.

Bwana Crépeau amesema anasikitishwa na mapendekezo ya Ulaya kwa sababu yanahusu kuwafukuza wahamiaji kwa halaiki, bila kufanya tathmini mwafaka kwa kila mmoja kwa kufuata utaratibu wa utoaji hifadhi, na hivyo kukiuka mikataba ya haki za binadamu ya Ulaya na kimataifa.