Tunataka dunia ya wanawake, watoto na barubaru kustawi siyo tu kuishi- Ban
Mkutano wa 60 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani ukiendelea kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema mkakati wa kimataifa wa afya ulioboreshwa utachochea kasi ya ustawi wa afya katika miaka 15 ijayo.
Akizungumza kwenye moja ya matukio ya kando ya mkutano huo wa kamisheni ya hali ya wanawake, Ban amesema mkakati huo una mpango wa kati wa miaka mitano wa kuwezesha ufanikiwe na kwamba..
“Mkakati huu unalenga dunia ambayo kwayo kila mwanamke, kila mtoto na kila barubaru siyo tu anaishi bali anachanua. Dunia ambayo kwayo watabadilika na kufikia ustawi wa kiwango cha juu kabisa.”
Hata hivyo Katibu Mkuu amesema uongozi thabiti wa kisiasa ni muhimu kufanikisha mpango huo akigusia jopo la ngazi ya juu alilounda mapema mwaka huu kwa lengo la kufanikisha afya duniani.
Amesema kinachohitajika pia ni fedha na ndio maana mwaka jana walianzisha mpango wa dunia wa kusaidai afya ya kila mama na kila mtoto na hadi sasa wahisani wameahidi zaidi ya dola Bilioni 25 kwa miaka mitano ijayo.