Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kauli baada ya ziara ya Sahara Magharibi, maafisa wa UM na Morocco katika mashauriano

Kauli baada ya ziara ya Sahara Magharibi, maafisa wa UM na Morocco katika mashauriano

Maafisa wa ngazi ya juu wa Umoja wa Mataifa na wale wa serikali ya Morocco wamekuwa na mawasiliano tangu jana kufuatia taarifa ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon baada ya mazungumzo yake na waziri wa Mambo ya nje wa Morocco Salaheddine Mezouar mjini New York, Marekani.

Katika taarifa hiyo Ban alielezea kutambua sintofahamu iliyoibuka kuhusiana na matumizi yake ya neno ukaliwaji kwa suala la Sahara Magharibi baada ya ziara yake eneo hilo, akisema ni mtazamo wake baada ya kushuhudia hali mbaya ya kibinadamu ambamo wakimbizi wa Sahrawi wameishi kwa muda mrefu.

Akijibu swali la waandishi wa habari waliotaka ufafanuzi zaidi juu ya taarifa hiyo, Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema.

(Sauti ya Dujarric)

“Katibu Mkuu katika ziara za karibuni amekuwa akichukua hatua kwa mamlaka ya Baraza la Usalama,ili kumwezesha yeye kufanikisha mashauriano. Bila shaka anasikitishwa kuwa kumekuwepo na sintofahamu juu ya matumizi ya neno Ukaliwaji. Kumekuwepo na mawasliano kati ya maafisa waandamizi wa Umoja wa Mataifa na wale wa Morocco tangu jana usiku baada ya kutolewa kwa taarifa.”

Katika taarifa hiyo pia Ban alieleza mshangao wake kwa taarifa ya karibuni ya serikali ya Morocco sanjari na kusikitishwa na maandamano ya Jumapili yaliyomlenga yeye binafsi. Amesisitiza kuwa vitendo kama hivyo dhidi yake ni ukosefu wa heshima kwake yeye binafsi na Umoja wa Mataifa.

Katibu Mkuu amerejelea wito wake wa tarehe Nne Novemba mwaka 2015 wa kutaka mashauriano ya dhati na makini bila masharti yoyote ili kusongesha mbele mchakato wa suluhu ya Sahara Magharibi.