Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 5 ya vita Syria, mashirika 102 ya kibinadamu yataka kuwezeshwa kufikia wahitaji

Miaka 5 ya vita Syria, mashirika 102 ya kibinadamu yataka kuwezeshwa kufikia wahitaji

Mashirika 102 ya kibinadamu yametoa wito wa kuwezesha ufikishaji wa usaidizi wa kibinadamu kwa Wasyria wote bila vikwazo au masharti, ikiwa leo ni miaka mitano tangu mzozo wa Syria kuanza.

Katika taarifa ya pamoja iliyotiwa saini na wawakilishi wao, mashirika hayo yamesema sasa kuna matumaini mapya ya amani kufuatia pande kinzani kuanza tena mazungumzo, na kukomesha taabu ya mamilioni ya watu wasio na hatia.

Mashirika hayo yametaka wawezeshwe wahudumu wa afya kufanya tathmini ya hali ya raia katika jamii zote na kuwatibu wagonjwa na majeruhi bila vikwazo, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wanayoihitaji kwa dharura, kama inavyotakiwa kulingana na sheria za kimataifa, na kusaidia katika utoaji wa chanjo kwa watoto kote nchini.