Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miaka 5 tangu mzozo wa Syria kuanza, Ban ataka hatua zaidi

Miaka 5 tangu mzozo wa Syria kuanza, Ban ataka hatua zaidi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema athari za kimataifa za kushindwa kuutanzua mzozo wa Syria ni dhahiri, akitaja haja ya juhudi mpya za kidiplomasia kikanda na kimataifa ili kuupatia suluhu mzozo huo.

Katika taarifa ya kuadhimisha miaka mitano tangu mzozo wa Syria kuanza, Ban ameelezea masikitiko yake kuwa, serikali ya Syria haikuitikia malalamiko halali ya watu wake kwa njia ya amani kupitia mazungumzo na mabadiliko serikalini, na kwamba wadau wa kikanda na kimataifa hawakuungana ili kuisaidia Syria kuimarika, na badala yake wakaitumia kama uwanja wa ushindani wa kikanda na wa kimataifa.

Hata hivyo, Katibu Mkuu ameelezea matumaini yake kufuatia kuundwa kwa kundi la kimataifa la kuisaidia Syria (ISSG), na ahadi za wanachama wake kutumia ushawishi wao kwa pande kinzani ili kuwezesha ufikishaji misaada kwa walengwa waliozingirwa au walioko katika maeneo magumu kufikia.

Ban amesema sasa diplomasia imebadilisha maisha ya kila siku ya Wasyria ambao wameteseka kwa muda mrefu, kwani ghasia zimepungua kwa kiwango kikubwa katika wiki mbili zilizopita, na kwamba watu wa Syria wamerejea tena mitaani, wakiandamana kwa amani kama ilivyokuwa miaka mitano iliyopita.

Aidha, Katibu Mkuu amesema ingawa anakaribisha mabadiliko haya, pekee hayawakilishi suluhu kamilifu kwa mzozo wa Syria, ambalo amesema linaweza kutokana tu na muafaka wa kisiasa unaoshughulikia matakwa halali ya watu wa Syria, na usitishaji mapigano kote nchini.