Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu milioni 12 hufariki dunia kila mwaka sababu ya mazingira duni

Zaidi ya watu milioni 12 hufariki dunia kila mwaka sababu ya mazingira duni

Shirika la Afya Duniani linakadiria kuwa watu wapatao milioni 12.6 wanafariki dunia kila mwaka kwa sababu ya kuishi kwenye mazingira yasiyokuwa salama kwa afya, ikiwa ni robo ya vifo vyote duniani. Taarifa zaidi ya Priscilla Lecomte.

(Taarifa ya Priscilla)

Vifo hivyo vimesababishwa na hatari zitokanazo na mazingira, zikiwa ni pamoja na uchafuzi wa hewa, maji na ardhi, kemikali, miyonzi ya nyuklia, na mabadiliko ya tabianchi.

Ripoti imesema vifo vyatokanavyo na uchafuzi wa hewa vimeongezeka hadi kufika sasa theluthi mbili ya vifo hivyo vyote.

Wakati huo huo vifo vilivyosababishwa na mifumo duni ya maji safi na usafi kama vile ugonjwa wa kuhara na malaria, vimepungua kutokana na uwekezaji katika mifumo hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Umma ya WHO  Maria Neira amesema kwamba cha kusikitha ni kwamba magonjwa hayo yanaweza kuzuiliwa.

(Sauti ya Bi Neira)

“Tukiwekeza katika harakati za msingi za kinga, maanake tukiondoa hatari hizo za kimazingira, basi tutapata fursa kubwa kwa afya ya umma, tukishawishi wale wanaowekeza kuendelea kuweka afya juu kwenye ajenda ya maamuzi yao.”