Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malawi kufungua kambi ya zamani idadi ya wakimbizi wa Musumbiji inapoongezeka

Malawi kufungua kambi ya zamani idadi ya wakimbizi wa Musumbiji inapoongezeka

Shirika la Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR), limekaribisha uamuzi wa serikali ya Malawi kufungua tena kambi ya zamani ya wakimbizi ili kusaidia kukabiliana na idadi inayoongezeka ya watu wanaokimbia kutoka Musumbiji.

Kwa mujibu wa UNHCR, takriban wakimbizi 10,000 kutoka Musumbiji wamesajiliwa kufikia sasa kusini mwa Malawi.

UNHCR imesema wengi wa watu wanaowasili upya wamekuwa wakivuka mpaka na kuingia Malawi tangu Disemba mwaka jana, na wapo katika kijiji kimoja kiitwacho Kapise, yapata kilomita 100 kusini mwa mji mkuu, Lilongwe, na wengine wamesambaa katika wilaya jirani ya Chikwawa. Leo Dobbs ni msemaji wa UNHCR, Geneva..

“Hadi sasa, watu 9,600 wamesajiliwa na UNHCR na serikali, lakini wengine bado wanasubiri kusajiliwa, na idadi nzima wakiwemo hao, ni takriban 11,500. Idadi ya watu wanaowasili kila siku imekuwa ikipanda tangu mwezi uliopita. Kutoka watu 130 mwishoni mwa Februari, sasa tunaona watu wapatao 250 wakiwasili kila siku Kapise.”