Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali ya haki za binadamu yazidi kuwa mbaya nchini DPRK

Hali ya haki za binadamu yazidi kuwa mbaya nchini DPRK

Serikali ya Jamhuri ya Watu wa Korea, DPRK, inaendelea kubinya haki za binadamu za raia wake na kudhibiti maisha yao yote, ameeleza leo mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu nchini humo, Marzuki Darusman.

Bwana Darusman ameongeza kwamba jamii ya kimataifa inapaswa kuhakikisha kwamba Rais wa DPRK, Kim Jong Un na viongozi wengine wanawajibishwa kwa uhalifu wa kibinadamu unaotekelezwa nchini humo.

Amesema hayo akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu mjini Geneva, Uswisi, akieleza kwamba watu wanaendelea kutumikishwa kama watumwa nchini humo, huku familia nzima zikikamatwa na kufungwa bila sababu.

Aidha Bwana Darusman ameongeza kwamba kiasi kikubwa cha pesa kinawekezwa na serikali katika kuunda silaha na makombora za nyuklia, huku idadi kubwa mno ya raia wakikumbwa na njaa.

Korea Kaskazini kwa upande wake haikutoa maoni kuhusu ripoti hiyo, kufuatia uamuzi wake wa kutohudhuria tena mikutano ya Baraza la Haki za Binadamu.