Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wazidi kukimbia Eritrea kwa hofu ya kulazimishwa kuhudumia jeshi milele

Vijana wazidi kukimbia Eritrea kwa hofu ya kulazimishwa kuhudumia jeshi milele

Mratibu Maalum kuhusu Hali ya haki za binadamu nchini Eritrea, Sheila Keetharuth, ameelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya maelfu ya watoto wa Eritrea waliokimbia nchi yao na kuvuka mipaka ya kimataifa bila kuandamana na mzazi au mlezi.

Bi Keetharuth amesema hayo akiwasilisha ripoti yake mbele ya Baraza la Haki za Binadamu leo, mjini Geneva, Uswisi.

Amesema chanzo cha tatizo hilo ni ukosefu wa fursa za elimu na kazi nchini mwao, pamoja na kiwango kikubwa cha ukiukwaji wa haki za binadamu, hasa sheria inayolazimisha vijana kujiunga na huduma za kijeshi kwa kipindi cha muda usiojulikana, wengine milele, licha ya serikali ya Eritrea kutoa ahadi ya kupunguza muda huo hadi miezi 18 tu.

(Sauti ya Bi Keetharuth)

Wengi wa wavulana na wasichana niliowahoji wenye umri wa kati ya miaka 12 na 17 wamesema kulazimishwa kujiunga na jeshi kumekuwa sababu ya msingi ya kukimbia nchi. Pia wanahofia kufungwa na kuteswa, wakiwa wameishuhudia kwenye jamii zao, hasa wakikwepa huduma ya kijeshi ya kitaifa.”   

Kwa upande wake mwakilishi wa Eritrea kwenye Baraza hilo amekanusha ripoti hiyo akisema kwamba raia wa Eritrea wanafurahia haki zao nchini humo.