Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanawake washirikishwe zaidi katika mabadiliko ya tabianchi : Waziri Ummy

Wanawake washirikishwe zaidi katika mabadiliko ya tabianchi : Waziri Ummy

Bara la Afrika na hasa wanawake ndio wanaobeba mzigo zaidi wa madhara ya mabadiliko ya tabianchi, huku wakinyimwa fursa ya kushiriki katika kutafuta suluhu kwa tatizo hilo, ameeleza leo Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Masuala ya wanawake, wazee na watoto wa Tanzania.

Bi Mwalimu amesema hayo akihutubia kikao cha 60 cha Kamisheni ya Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya wanawake, CSW60 kwa niaba ya kundi la nchi za Afrika, akisisitiza umuhimu wa kushirikisha zaidi wanawake katika uongozi wa kimataifa kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, amesema hayo hayatoshi.

(Sauti yaUmmy)

“Wanawake wanapaswa kuweza kuongoza katika ngazi za kitaifa na serikali za mitaa. Ubunifu wao, ujuzi wa kiasili, matarajio yao yanaweza kusaidia katika kubuni na kushawishi suluhu kuhusu mabadiliko ya tabianchi."

Aidha amezungumzia suala la kilimo ambacho hushughulisha wanawake zaidi, akisema la msingi ni kusaidia sekta binafsi ili kukuza ukuaji wa uchumi katika sekta hiyo na hivyo kuwezesha wanawake.