Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama kwa kauli moja lapitisha azimio dhidi ya ukatili wa kingono

Baraza la Usalama kwa kauli moja lapitisha azimio dhidi ya ukatili wa kingono

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja limepitisha azimio linalounga mkono hatua za Katibu Mkuu wa umoja huo Ban Ki-moon dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kingono vinavyotekelezwa na walinda amani wa chombo hicho.

Azimio hilo mathalani linaridhia uamuzi wa Katibu Mkuu wa kurejesha makwao vikosi ambavyo vitathibitishwa pasipo shaka kuhusika na vitendo hivyo.

Halikadhalika linamtaka Katibu Mkuu kubadilisha vikosi husika iwe jeshi au polisi husika iwapo nchi yao haijachukua hatua yoyote za kuwajibisha.

Azimio hilo linasema iwapo nchi  ambayo vikosi vyake vinahusika na vitendo hivyo haikuchukua hatua husika, basi Katibu Mku atathmini ushiriki wa nchi hiyo kwenye operesheni za baadaye za ulinzi amani.

Wajumbe pia wameridhia suala la walinda amani kuchunguzwa kabla ya kwenda kwenye operesheni halikadhalika usaidizi kwa wahanga.

Katika azimio hilo wamesema wametambua kuwa ni vyema kuchukua hatua ili watendaji wachache wanaoshiriki vitendo hivyo wasichafue kazi nzuri inayofanywa na watendaji wengine.