Vuta nikuvute Barazani, nani awajibike na ukatili wa kingono?

Vuta nikuvute Barazani, nani awajibike na ukatili wa kingono?

Alhamisi ya tarehe 10 Machi mwaka 2016, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon aliwasilisha mbele ya Baraza la Usalama hatua mahsusi za kukabiliana na ukatili wa kingono unaofanywa na walinda amani wa umoja huo.Mikakati hiyo inagusa maeneo makuu matatu kutokomeza ukwepaji sheria kwa wakosaji, kusaidia wahanga wa vitendo hivyo na kuimarisha uwajibikaji kama njia ya kuzuia vitendo hivyo.

Ban akafunguka kuhusu vitendo hivyo..

(Sauti ya Ban)

“Vinadidimiza uaminifu kati ya Umoja wa Mataifa na wanufaika! Vinasaliti maadili na misingi ambayo kwayo Umoja wa Mataifa unalenga kusongesha! Vinachafua uhalali wa operesheni za ulinzi wa amani za Umoja wa Mataifa na Umoja wa Mataifa kwa ujumla.”

Ban akaenda mbali zaidi kutetea msimamo wake wa hatua akisema..

(Sauti ya Ban)

“Ndani ya nyumba! Nafikiri ni lazima tujisafishe kwamba na ndipo naweza kutoka nje na kuambia nchi wanachama zitokomeza ukatili wa kingono dhidi ya wanawake.”

Naibu Mwakilishi wa Pakistani kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Nabil Munir akawa na mtazamo tofauti..

(Sauti ya Balozi Munir)

“Nchi mwanachama au kikosi kizima hakipaswi kuwajibika kwa uhalifu wa mtu mmoja. Kutofautisha kati ya kosa na tuhuma ni muhimu na lazima izingatiwe. Mwelekeo wa sasa inaonekana kuwa kwenye tuhuma. Wito wa ujumla kwa nchi kutathmini taratibu zake za jinai na sheria ni lazima uepukwe.”

image

Hata hivyo Samantha Power, Mwakilishi wa kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa akasema..

(Sauti ya Balozi Power)

“Sote tunakubali hakuwezi kuwepo kwa kosa la pamoja au unyanyapaa wa Taifa. Nafikiri hiyo ni muhimu sana. Nadhani sote tunajaribu kuweka hilo bayana taarifa zetu. Lakini ndio maana wajibu wa mtu mmoja mmoja, kuchukuliwa hatua mtu mmoja au kuadhibiwa mtu mmoja iwapo litapatiwa hakikisho ni muhimu sana. Na hili halifanyiki.”

Na kutokana na vuta ni kuvute juu ya nini chakufanya wakati watoto na wanawake wanazidi kukumbwa na madhila ya ukatili wa kingono, balozi Power akafunguka..

(Sauti Balozi Power)

“Iwapo ukatili huo ungalifanyiwa watoto wetu, tusingalikuwa kuwa hapa tunabishana juu ya mamlaka ya hatua namna hii. Tusingaliwaza kuhusu.. ooh hiki kiko hapa au hiki ni cha pale, La hasha! Lakini kwa kuwa wanafanyiwa watoto wa wengine, tunajaribu kulisukumu jambo hili kwigineko, ambako tunajua kabisa huko litakumbwa na mkwamo na litasalia kama lilivyo na ni katika ulimwenguni ambako hakutakuwa na mabadiliko kwa wahanga.”

image