Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Utekelezaji wa ajenda 2030 kuwa kitovu cha ajenda za #CSW60 New York

Utekelezaji wa ajenda 2030 kuwa kitovu cha ajenda za #CSW60 New York

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake, UN Women Phumzile Mlambo-Ngcuka amesema mkutano wa 60 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW utakaoanza Jumatatu ijayo utajikita kwenye utekelezaji wa ajenda ya maendeleo endelevu 2030.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini New York, Marekani, Bi. Mlambo-Ngcuka amesema wataangazia uhusiano wa uwezeshaji wanawake na ajenda hiyo kwa kuzingatia kwamba tafiti zimebaini uhusiano chanya kati ya uwezeshaji wanawake na maendeleo ya  jamii.

Mathalani amenukuu tafiti zinazoonyesha kuwa pato la ndani la dunia litaongezeka na kufikia dola Trilioni 28 mwaka 2025 iwapo wanawake watajumuika kwenye soko la ajira sawa na wanaume.

Halikadhalika amezungumzia jukwaa la vijana ndani ya kamisheni ya hali ya wanawake akisema linaanza kesho na ni kwa mara ya kwanza kabisa likiangazia vijana na usawa wa kijinsia ambapo..

(Sauti ya Mlambo-Ngcuka)

“Jukwaa hilo litatoa fursa ya kihistoria kwa vijana kukutana pamoja na kupazia sauti masuala yanayowahusu.  Kwa mara ya kwanza kabisa kutakuwepo na hoja zilizopitishwa vijana ambazo zitakuwa ni mwongozo kwa vikao vingine vya CSW na majumuisho yatawasilishwa wakati wa mkutano mkuu wa kamisheni ya hali ya wanawake, CSW.”

Bi. Mlambo-Ngucka amesema mkutano huo wa ngazi ya juu ukitarajiwa kumalizika tarehe 24 mwezi huu ambapo zaidi ya mashirika ya kiraia 1000 yamesajili wawakilishi zaidi ya 8,100 kwenye mkutano huo utakaohusisha pia wawakilishi wa serikali.