Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usindikaji duniani wabaki mdogo chumi zinazoibuka zinapodidimia- UNIDO

Usindikaji duniani wabaki mdogo chumi zinazoibuka zinapodidimia- UNIDO

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu viwanda na maendeleo, (UNIDO), limesema leo katika ripoti yake kuwa mwendo wa ukuaji wa uzalishaji katika sekta ya usindikaji ulipungua katika miezi mitatu ya miwsho ya 2015, kufuatia ukuaji katika chumi zinazoendelea na zinazoibuka kuwa hafifu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baada ya kuimarika kwa muda mfupi katika miezi mitatu ya kwanza ya 2015, uzalishaji katika sekta ya usindikaji duniani ulipanda kwa asilimia 1.9 tu katika kipindi cha miezi mitatu ya mwisho mwaka huo.

Ripoti hiyo imesema ukuaji mdogo ulishuhudiwa pia Ulaya na Amerika Kaskazini, na kwamba kufuatia kuimarika kwa thamani ya dola ya Kimarekani, bidhaa za usindikaji zinazouzwa nje kutoka Marekani zilipungua.

Aidha, ukuaji mdogo wa uchumi wa Uchina uliathiri kiwango cha bidhaa zinazoagizwa na Wachina kutoka Ulaya, huku uzalishaji wa usindikaji barani Afrika ukishuka kwa asilimia 0.2, hasa kwa sababu ya Afrika Kusini ambayo ndiyo inaongoza katika usindikaji Afrika.