Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ni muhimu tuwekeze kwenye kudhibiti majanga ya afya: UNISDR, WHO

Ni muhimu tuwekeze kwenye kudhibiti majanga ya afya: UNISDR, WHO

Mlipuko  wa virusi vya Ebola na Zika umeonyesha umuhimu wa uwekezaji katika kukabiliana na majanga ya afya imesema taarifa ya pamoja ya Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kupunguza majanga UNISDR na shirika la afya ulimwenguni WHO. Grace Kaneiya na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA GRACE KANEIYA)

Mashirika hayo yametaka mashirika ya kitaifa ya kudhibiti majanga kuendeleza maandalizi  na uwezo wa kukabili majanga kwa kujumuisha afya.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, kando mwa majanga kama vile mafuriko, matetemeko na vimbunga, majanga ya afya yanapaswa kupewa kipaumbele mathalani mlipuko wa Ebola uliokumba Afrika Magharibi na mlipuko wa Zika.

Mkuu wa UNISDR Robert Glasser amesema ni muhimu kushugulikia majanga yote ya kibinadamu na yale ya asili na majanga yatokanayo na mazingira, teknolojia na kibayolojia.

Amesema licha ya ukweli kwamba kuna udhibiti imara wa majanga yatokanayo na matetemeko na matukio mengine yatokanayo na hali ya hewa ambayo huathiri zaidi ya watu milioni 100 duniani kila mwaka, uwezo huo lazima uelekezwe katika afya ambapo msukumo ni virusi kama vya Zika.