Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutia saini mikataba pekee haitoshi, itekelezwe kwa dhati- Zeid

Kutia saini mikataba pekee haitoshi, itekelezwe kwa dhati- Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadam Zeid Ra’ad Al Hussein ameeleza wasiwasi wake kuhusu kitendo cha nchi kutia saini na kuridhia mikataba ya haki za binadamu bila kutekeleza kwa dhati.

Amesema hayo wakati akiwasilisha ripoti yake ya mwaka mbele ya Baraza la Haki za binadamu la Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

Amesema kusaini na kuridhia mikataba hiyo pekee bila bila kuchukua hatua za dhati kuitekeleza siyo mafanikio, akiongeza kuwa ni lazima kuwepo kwa ufuatiliaji na mabadiliko ya dhati ili hatua hizo ziweze kuleta  uhuru zaidi na utu kwa wananchi husika.

Zeid amesema haki za binadamu si suala la kuweka alama ya vema kuwa imeridhiwa ili kukuza taswira ya nchi kimataifa bali inapaswa kuleta mabadiliko ya kweli.

Ripoti hiyo pia imeangazia mizozo inayoendelea maeneo mbali mbali duniani kama vile Jamhuri ya Afrika ya Kati, suala la wakimbizi wanaosaka hifadhi Ulaya na ukatili wa kingono unaotekelezwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa.