Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

El Nino na mizozo vyasababisha nchi kuhitaji misaada ya chakula

El Nino na mizozo vyasababisha nchi kuhitaji misaada ya chakula

Idadi ya nchi zinazohitaji msaada wa chakula duniani sasa imeongezeka na kufikia 34 ikiwemo 27 za Afrika, El Nino ikitajwa kuwa sababu ya kupungua kwa uzalishaji.

Hiyo ni kwa mujibu wa ripoti ya hali ya chakula na mwelekeo wake duniani iliyotolewa leo na shirika la chakula na kilimo duniani, FAO, ikisema ni ongezeko kutoka 33 mwezi Disemba mwaka jana baada ya Swaziland nayo kujumuishwa.

FAO imesema matarajio ya uzalishaji kwenye kilimo yamepungua Kusini mwa Afrika kutokana naEl Nino ilihali huko matarajio ya mavuno huko Morocco na Algeria yamepunguzwa kutokana na hali ya ukame.

Hata hivyo kwa nchi kama vile Iraq, Syria, Yemen, Somalia, na Jamhuri ya Afrika ya Kati mapigano na mizozo yamekuwa mwiba kwa sekta ya kilimo na hivyo kuzidi kukomaza janga la kibinadamu kwenye nchi hizo.

Kwingineko mathalani Ulaya, majira ya baridi yanatoa neema kwa mazao ya msimu huo huku makadirio ya mavuno ya ngano  huko Asia kwa mwaka huu yakitia moyo.