Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UM watoa kanuni mpya za kupunguza ajali za magari yanayotumia nishati ya umeme

UM watoa kanuni mpya za kupunguza ajali za magari yanayotumia nishati ya umeme

Hatari ya magari yanayotumia nishati ya umeme, au ‘magari kimya’ sasa itapunguzwa, kufuatia kanuni mpya zilizoafikiwa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa Ulaya, UNECE, zikitaka magari hayo yawe na vitoa onyo kwa sauti. Taarifa kamili na Joshua Mmali.

(Taarifa ya Joshua)

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kufuatia kongamano la kimataifa la kudhibiti kanuni za magari, magari ya miundo mseto na yanayotumia nishati ya umeme, hayatoi mgurumo wa injini.

Taarifa hiyo imesema kutokuwa na mgurumo kunasaidia kuboresha afya na maisha kwa kupunguza kelele zinazotokana na mwendo wa magari, lakini wakati huo huo ni hatari kwani magari hayo hayatoi onyo lolote kwa watu wanaosafiri kwa miguu.

Kanuni hizo zilizotolewa zimependendekeza kuweka chombo cha kutoa kelele au mgurumo katika injini za magari hayo, ili zisaidie kuokoa maisha ya watu wenye ulemavu wa kuona, waendesha baiskeli na watembea kwa miguu.