Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kitivo cha chuo kikuu chazinduliwa Kakuma: UNHCR

Kitivo cha chuo kikuu chazinduliwa Kakuma: UNHCR

Kitivo kipya cha chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Masinde Mulira (MMUST) kimezinduliwa kwenye kambi ya wakimbizi ya Kakuma nchini Kenya, kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudhumia Wakimbizi UNHCR.

Mwakilishi wa UNHCR nchini Kenya Raouf Mazou aliyehudhuria uzinduzi huo pamoja na wakuu wa chuo kikuu, amesema kitivo hicho kitawapatia wakimbizi na jamii zinazowapokea fursa za elimu ya ngazi za juu.

Tayari UNHCR inashirikiana na MMUST katika kuwasomesha wakimbizi na watu kutoka jamii jirani ambapo wakati wa uzinduzi huo wanafunzi 43 wamepatiwa diploma ya elimu.

Aidha UNHCR imeeleza kwamba Kituo cha Walimu kimezinduliwa pia sanjari na uzinduzi huo, ambacho kinawapatia walimu wote wa kambi nyenzo za kujisomesha kupitia TEHAMA na mtandao wa intanet unaoletwa kituoni hapo kupitia nishati ya jua.