Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN Women kuanzisha mafunzo kwa wanawake wagombea DR Congo

UN Women kuanzisha mafunzo kwa wanawake wagombea DR Congo

Shirika la Umoja wa Mataifa la Wanawake UN women nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC litaanzisha mwaka huu mafunzo maalum kwa ajili ya wanawake wanaotarajia kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi kwenye uchaguzi wa wabunge utakaofanyika Novemba mwaka huu. Taarifa zaidi na Flora Nducha

(TAARIFA YA FLORA)

Mwakilishi wa UN Women nchini DRC, Francoise Ngendahayo amesema hayo leo akizungumza na waandishi wa habari mjini Kinshasa akisema ni mpango wa shirika hilo katika kusaidia kufikia usawa wa kijinsia nchini humo.

Bi. Ngendahayo amesema kwamba UN women itasaidia wanawake wote watakaogombea nafasi kwenye uchaguzi ujao na kuwezesha waliochaguliwa tayari kufundisha wagombea wenzao.

(Sauti ya Bi Ngendahayo)

“ Pia tutahamasisha wakuu wa vyama vya kisiasa, ili waweke wanawake kwenye orodha za wagombea, kwa kuheshimu katiba ambayo ni wazi sana kuhusu uwiano wa hamsini kwa hamsini, lakini ambayo haikuweka wazi harakati za utekelezaji wake.”

Amesema jitihada hizo ni moja ya hatua zitakazochukuliwa na UN Women kusaidia serikali ya DRC kuendeleza usawa wa kijinsia na kufikia uwiano wa hamsini kwa hamsini kwenye kila sekta ya jamii.