Kuna uhusiano baina ya uhalifu na unyanyasaji kwa walio wachache:UM

Kuna uhusiano baina ya uhalifu na unyanyasaji kwa walio wachache:UM

Ubaguzi na unyanyasaji wa wanawake, wasichana na walio wachache ni lazima uonekane kama ulivyo, yaani utesaji, amesema  leo mtaalamu wa haki za binadamu.

Juan Mendez, ambaye ni mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu masuala ya utesaji amesema mateso kwa wanawake na wasichana, wakiwemo mashoga , wanaofanya mapenzi ya jinsia moja, waliobadili jinsia na wanaoshiriki mapenzi ya jinsia zote (LGBT), yanaendelea kuchukuliwa kama kitu cha kawaida, kuliko unyanyasaji katika  nchi nyingi.

Katika ripoti yake ya tano na ya mwisho kwenye baraza la haki za binadamu Bwana Mendez ameelezea kushindwa kwa sheria za kimataifa kuwalinda wanawake, wasichana na walio wachache kutokana na mateso na vitendo vya kikatili. Ameongeza kuwa unyanyasaji ni dhahiri kwa watu wa LGBT

(SAUTI YA MENDEZ)

“Kuna angalau nchi 76 duniani ambazo zina sheria zinachukulia kuwa ni uhalifu kushiriki mapenzi ya jinsia moja kwa watu wazima hata kama ni kwa faragha. Tunadhani kuna uhusiano baina ya kuharamisha ushoga, ushiriki wa mapenzi ya jinsia moja, kubadili jinsia na ghasia na unyanyapaa ambao unalikabili kundi la watu hawa.”

Ameongeza kuwa ubaguzi utakonao na jinsia upo sasa karibu katika kila utamaduni wa kila jamii. Amegusia pia suala la ndoa za utotoni ambazo zinaathiri wanawake bilioni moja, huku milioni 250 waliolewa kabla ya kutimiza umri wa miaka 15.