Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tunaweza tu kushughulikia changamoto zinazowakumba wanawake kwa kuwawezesha- Ban

Tunaweza tu kushughulikia changamoto zinazowakumba wanawake kwa kuwawezesha- Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, amesema changamoto nyingi zinazowakabili wanawake duniani zinaweza kushughulikiwa tu iwapo wanawake watawezeshwa kama mawakala wa mabadiliko.

Ban amesema hayo katika ujumbe wake kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, leo Machi 8.

Akitaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo, Katibu Mkuu amesema, katika maeneo maskini duniani, wanawake bado wanakumbana na hatari ya kufariki wanapojifungua, watoto wa kike wanakeketwa, wasichana wanavamiwa na kubakwa wanapokwenda shule, miili ya wanawake inatumiwa kama nyanja za mapigano vitani, na kwamba wajane wanatelekezwa na kufanywa fukara.

Ban amesema anatiwa uchungu siku hii akiona wanawake na wasichana wananyimwa haki zao, lakini anatiwa moyo na watu wanaochukua hatua kila mahali wakijua kuwa kuwezesha wanawake kunachangia kuendeleza jamii.

Aidha, Katibu Mkuu ametoa wito wa kuwekeza fedha, uchagizaji, na utashi wa kisiasa katika kufikia usawa wa jinsia, akisema kuwa hakuna uwekezaji bora zaidi katika mustakhbali wetu wa pamoja kuliko huo.