Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FAO, IFAD, WFP na IDLO zapaazia usawa sauti usawa kuadhimisha Siku ya Wanawake

FAO, IFAD, WFP na IDLO zapaazia usawa sauti usawa kuadhimisha Siku ya Wanawake

Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa yaliyoko jijini Roma, Italia, wamekutana leo kumulika ufanisi uliopatikana na fursa zilizopo katika kufikia usawa wa jinsia, wakikubaliana kuwa kuongeza kasi ya kuwezesha wanawake kila mahali ni muhimu katika kutokomeza njaa na kufikia malengo mapya ya maendeleo endelevu.

Mjadala huo wa ‘Sayari 50:50: Imarisha nguvu kwa usawa wa Jinsia na kutokomeza njaa’ , umeandaliwa na Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Shirika la Mfuko wa Kimataifa kwa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP), na Shirika la Kimataifa la Sheria ya Maendeleo (IDLO).

Katika hafla hiyo ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wakuu wa mashirika hayo wamesema, kujenga ubia mpana ni muhimu katika kutekeleza na kuimarisha kasi inayohitajika katika kufikia malengo ya kimataifa ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030, likiwemo lengo la usawa wa jinsia.

Mkuu wa WFP, Ertharin Cousin, amekumbusha washiriki kuwa kuimarisha nguvu za kuwezesha wanawake na usawa wa jinsia, siyo tu suala muhimu kimaadili, lakini pia ni muhimu katika kutokomeza umaskini, kwani wakipewa fursa, wanawake watapata ufanisi  mkubwa na familia na jamii zao zitanawiri.