Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wazidi kuwa wahanga wa ukatili CAR: ripoti

Watoto wazidi kuwa wahanga wa ukatili CAR: ripoti

Ripoti mpya ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu ukatili dhidi ya watoto nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati CAR inaonyesha kuwa watoto wamekuwa wahnaga wa kiwango kikubwa cha ukatili na ghasia nchini humo, huku ukwepaji wa sheria ukienea na mamlaka za serikali zimesambaratika.

Vitendo hivyo vimeshuhudiwa katika ya mwaka 2011 na 2015, Umoja wa Mataifa ukiwa umepokea ripoti ya mauaji 333 ya watoto, mengi yakiwa ni kwa misingi ya ukabila, dini au ulipizaji kisasi, huku visa zaidi ya 500 vya ubakaji vikiripotiwa.

Aidha kwa mujibu wa ripoti hii iliyotolewa leo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF limekadiria kuwa watu 6,000 hadi 10,000 wametumikishwa vitani. Wengi wao bado wanatumikishwa na waasi licha ya watoto zaidi ya 5,500 kuachiliwa huru na vikundi vya kujihami kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu watoto kwenye mizozo Leila Zerrougui ametoa wito kwa wale wanaoweza kuleta mabadiliko nchini humo wachangie katika kusaidia watoto walioathirika na vita kupata huduma za elimu, afya na kurejeshwa kwenye jamii.