Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ili kufikia muskhbali tunaoutaka wanawake hawawezi kusalia nyuma: Mlambo-Ngcuka

Ili kufikia muskhbali tunaoutaka wanawake hawawezi kusalia nyuma: Mlambo-Ngcuka

Ili kufikia Muskhbali tunaoutaka hakuna mtu atakayeachwa nyuma, na ni lazima kuanza na wasio pewa kipaumbele ambao ni wanawake na wasichana, ingawa katika maeneo yenye umasikini na matatizo inajumuisha pia wavulana na wanaume.

Hayo yamesemwa na mkurugenzi mtendaji wa kitengo cha Umoja wa Mataifa cha masuala ya wanawake UN Women Bi Phumzile Mlambo-Ngcuka katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya wanawake.

Amesema wanawake na wasichana ni muhimu katika kutafuta suluhu endelevu ya changamoto za umasikini, kutokuwepo usawa, na kujikwamua katika jamii ambazo zimeathirika na vita, majanga, na wakimbizi wa ndani.

Ametoa wito wa kuchukua hatua kwa ajili ya usawa wa kijinsia “Step It Up for Gender Equality”

(SAUTI YA MLAMBO-NGCUKA)

“Jinsi gani tunaweza kuhakikisha wanawake hawabaguliwi katika uchumi kwa pamoja, kuchukua hatua kwa pamoja na serikali, sekta binafsi na jamii na kuhakikisha kwamba mapengo tulilyobaini katika tathimini yetu yanashughulikiwa, na ndio maana tunatoa wito kwa wanaume na wavulana kuwa sehemu ya suluhu huko ndio kuchukua hatua”

Pia amesistiza umuhimu wa ushiriki wa wanawake kama moja ya vigezo vya lazima kwa ajenda ya maendeleo endelevu ya mwaka 2030.