Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Elimu Bora ni Ubora wa jamii: Ban ki-moon

Elimu Bora ni Ubora wa jamii: Ban ki-moon

Akiwa ziarani Algeria, Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa Ban Ki-moon ametembelea shule ya msingi ya Mohamed Maazouzi iliyofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto UNICEF, na akasema elimu borani msingi wa jamii bora.

Akiwa ameambatana na Waziri wa Elimu wa Algeria bi Nouria Benghabrit Remaoun, Ban amesisitiza kwamba elimu bora ni kipaumbele kwa Umoja wa Mataifa katika kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu.

(sauti ya Bwana Ban)

“Ubora wa Elimu ndio ubora wa jamii. Tukiwapa watoto fursa za kujifunza, watakuwa raia wenye kipaji cha ubunifu na uzalishaji, na uwezo wa kuleta mabadiliko”

Ameongeza kwamba mashirika ya Umoja wa Mataifa yameridhika na ushirikiano wao na Wizara ya Elimu ya Algeria.

Kwa mujibu wa msemaji wa Umoja wa Mataifa, wizara ya elimu ya Algeria imejitahidi kuhakikisha watoto wote nchini humo wanapatiwa elimu bure ya msingi na sekondari.

Uandikishwaji wa watoto shuleni umeimarija sana nchini humo kwa kipindi cha miaka ishirini iliyopita, huku idadi ya watoto wenye umri wa zaidi ya miaka 10 wasiojua kuandika wala kusoma ikiwa imepungua kutoka kwa asilimia 72 na kufika asilimia 20.