Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNHCR yaaninisha hatua sita za kutatua mtafaruku wa wakimbizi Ulaya:

UNHCR yaaninisha hatua sita za kutatua mtafaruku wa wakimbizi Ulaya:

Katika maandalizi ya mkutano wa wakuu wa nchi za Muungano wa Ulaya na Uturuki uliopangwa kufanyika Machi 7 mjini Brussels Ubelgiji, shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limeaninisha mapendekezo yenye lengo la kusaidia kupata suluhu ya tatizo la wakimbizi barani Ulaya.

Kwa mujibu wa mkuu wa UNHCR Filippo Grandi wakati umetutupa mkono na uongozi thabiti na mtazamo imara unahitajika haraka kutoka kwa viongozi wa Muungano wa Ulaya kukabiliana na hali ya wakimbizi inayoweza kupata suluhu. Akiwaasa viongozi wote wa Muungano kuwa ushiriki wao katika kupata suluhu ni muhimu. .

Pia bwana Grandi amependekeza hatua sita kama muongozo wa kuelekea suluhu hiyo ikiwemo mosi utekelezaji wa mtazamo wa kuwahamisha waomba hifadhi kutoka Ugiriki na Italia, pili kuisaidia Ugiriki kukabiliana na dharura ya kibinadamu,

tatu kuhakikisha utekelezaji wa sheria za Muungano wa Ulaya kuhusu waoomba hifadhi, nne kuhakikisha njia salama za kisheria zinapoatikana kwa wakimbizi kusafiri Ulaya.

Tano kuwalinda walio katika hatari ikiwemo watoto wanaoingia bila walezi na sita kuanzisha mfumo maalumu wa uwajibikaji kwa waomba hifadhi ikiwemo vituo vya kuwaorodhesha.