Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watu wenye ulemavu bado wanatengwa na kunyanyapaliwa- mtaalam wa UM

Watu wenye ulemavu bado wanatengwa na kunyanyapaliwa- mtaalam wa UM

Mtaalam maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za watu wenye ulemavu, Catalina Devandas Aguilar, amesema watu wenye ulemavu bado wananyanyapaliwa na kutoshirikishwa katika utungaji sera, hata ikiwa sera hizo zinawahusu wao.

Akitoa ripoti kwa Baraza la Haki za Binadamu kuhusu ushiriki wa watu wenye ulemavu katika harakati za umma na kuchukua uamuzi, mtaalam huyo amesema ni nadra watu hao bilioni moja wenye ulemavu kuchukua nyadhfa serikalini, hata ingawa ni asilimia 15 ya idadi nzima ya watu duniani.

Mtaalam huyo wa haki za binadamu amekumbusha kuhusu mkataba kuhusu watu wenye ulemavu, ambao umeridhiwa nan chi 162, ukiziwajibisha serikali kuwashirikisha watu wenye ulemavu, kutambua haki yao ya kushiriki katika nyanja zote za uamuzi unaoathiri umma, na sio tu unaohusika na ulemavu wao. Licha ya mkataba huo, amesema hayo bado ni ndoto tu..

“Sauti zetu hazisikiki. Kutengwa kwetu ni hasara kwa jamii nzima. Na kunaenda kinyume na dhana ya ‘kutomwacha yeyote nyuma’. Tukiendelea hivi, hatuwezi kutimiza malengo ya maendeleo endelevu, watu wenye ulemavu wasipozingatiwa vinginevyo.”