Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban na Dlamini-Zuma waeleza kusikitishwa na mapigano mapya Darfur

Ban na Dlamini-Zuma waeleza kusikitishwa na mapigano mapya Darfur

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Muungano wa Afrika, AU, Nkosazana Dlamini-Zuma, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, wameeleza kutiwa wasiwasi mkubwa na kuchacha kwa mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Sudan na vikosi vya waasi wa Sudan Liberation Army/Abdul Wahid, katika eneo la Jebel Marra, jimbo la Darfur, na athari zake kwa raia.

Tangu kuanza ghasia wiki sita zilizopita, zaidi ya raia 90,000 wamelazimika kuhama makwao Darfur Kaskazini, ikizingatiwa kuwa tayari watu milioni 2.6 wamefurushwa makwao na mzozo wa Darfur.

Aidha, kuna ripoti ambazo hazijathibitishwa za idadi kubwa ya watu Darfur ya Kati kufurushwa makwao, ambayo haijaweza kuthibitishwa na mashirika ya kibinadamu kwa sababu ya ugumu wa kuwafikia.

Ban na Dlamini-Zuma wametoa wito kwa serikali ya Sudan kushirikiana kikamilifu na ujumbe wa Umoja wa Mataifa na Muungano wa Afrika Darfur, UNAMID, kuwezesha uhuru wa ujumbe huo kutembea, na wahudumu wa kibinadamu katika juhudi zao za kuwalinda na kuwasaidia raia walioathiriwa na mapigano.