Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hali Syria bado tete lakini kuna maendeleo- de Mistura

Hali Syria bado tete lakini kuna maendeleo- de Mistura

Mjumbe maalum wa Umoja wa Maifa kwa suala la Syria, Staffan de Mistura amesema makubaliano ya kusitisha mapigano nchini humo yanaendelea licha ya matukio madogo  ya ghasia ya hapa na pale.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi leo na waandishi wa habari, Bwana de Mistura amesema siku sita tangu makubaliano hayo baina ya pande kuu za upinzani, kiwango cha ghasia kimepungua  na hivyo kuwezesha misaada kufikia wahitaji waliokosa kwa muda mrefu.

(Sauti ya de Mistura)

“Kiwango cha ghasia kimepungua kwa kiasi kikubwa, hata ukiuliza wananchi wa Syria. Hii ni habari njema kwa wasyria. Kwa bahati mbaya bado kuna maeneo ambako kuna mapigano ikiwemo sehemu za Hama, Homs, Latakia na Damascus. Lakini yamedhibitiwa.”

Amepongeza Urusi na Marekani ambazo ni sehemu ya kikosi kazi kwa Syria, kwa kusaidia kudhibiti ghasia hizo zinazoibuka akisisitiza kuwa wanafuatilia kwa karibu na wameazimia suala la kumaliza chuki kutimia.

Hadi leo zaidi ya malori 230 yamefikia maeneo husika yakiwa na misaada kwa watu 115,000 ikiwemo wakazi wa mji wa Madamiyet ambako malori matatu yaliwasilisha misaada baada ya kuikosa kwa mwaka mmoja na nusu.

Kuhusu mazungumzo ya amani ya Syria yaliyopangwa kuanza tarehe Tisa mwezi huu, mjumbe huyo maalum amesema ni vyema pande husika zifahamu kuwa ni mazungumzo ya wazi yasiyowekewa ukomo.