Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Serikali zipiganie utokomezaji wa mabomu ya kutegwa ardhini- Kofi Annan

Serikali zipiganie utokomezaji wa mabomu ya kutegwa ardhini- Kofi Annan

Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, amesema leo kuwa jitihada za kupigania dunia isiyo na mabomu ya kutegwa ardhini zimepiga hatua kubwa tangu mkataba wa kimataifa wa Ottawa unaopiga marufuku mabomu hayo ulipoanza kutekelezwa mnamo mwaka 1999, lakini sasa wakati umewadia wa kuchukua hatua madhubuti za pamoja.

Bwana Annan amesema hayo akihutubia kongamano la kwanza la kutoa ahadi kuhusu utekelezaji wa mkataba wa kupiga marufuku mabomu yanayotegwa ardhini, akionya kuwa ni maeneo machache tu duniani ndiyo yasiyokuwa na mabomu hayo kufikia sasa.

“Mabomu ya kutegwa ardhini na mabaki ya vilipuzi vya vita bado ni tishio kubwa kwa maeneo mengi ya dunia, na uchungu na taabu inayosababishwa na mabomu haya, aghalabu huwakumba zaidi wanawake, watoto na watu wasio na hatia. Madhara yake ya kifo na majeraha huiathiri jamii muda mrefu baada ya mzozo kuisha.”

Takwimu za hivi karibuni zaidi za Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na mabomu ya kutegwa ardhini na vilipuzi, UNMAS, zinaonyesha kuwa kuna mamia ya maelfu ya wahanga wa mabomu hayo, wengi wao wakiwa raia na watoto, na kwamba kwa wastani, watu 10 huathiriwa na mabomu hayo kila siku.