Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNFPA, Iraq wazindua matokeo ya tathimini ya afya ya dharura ya uzazi na watoto

UNFPA, Iraq wazindua matokeo ya tathimini ya afya ya dharura ya uzazi na watoto

Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu(UNFPA) kwa kushirikiana na serikali ya Iraq wamezindua matokeo ya tathimini ya wizara ya afya ya nchi hiyo kuhusu afya ya dharura ya uzazi na watoto wachanga (EmONC) ambapo imebainika kuwa Iraq ina uhitaji mkubwa wa huduma za kuokoa maisha za afya ya uzazi kwa mama na mtoto.

Taarifa ya UNFPA inasema kuwa licha ya hatua kubwa zilizofikiwa na Iraq katika miaka ya hivi karibuni ambapo idadi ya vifo vya wanawake wajawazito imepungua, bado kuna changamoto kwani ni theluthi moja tu ya hospitali na hakuna vituo vya afya ambavyo vinazingatia viwango vya kimataifa vya EmONC

Kadhalika theluthi mbili ya wanaojifungua hujifungulia katika maeneo hayo yasiyo na huduma mujarabu, hatua inayohitaji serikali na jumuiya ya kimataifa kufanyia kazi suala hilo haraka.

Kwa upande wake mwakilishi wa serikali ya Iraq amesema maendeleo ya kudhibiti vifo vya akina mama waja wazito na watoto yanategemea uimarishwaji wa afya ya uzazi ikiwamo huduma za dharura za afya ya uzazi.