Skip to main content

Mamia ya raia wakimbia mashambulizi ya waasi Kivu Kaskazini DRC- MONUSCO

Mamia ya raia wakimbia mashambulizi ya waasi Kivu Kaskazini DRC- MONUSCO

Mashambulizi ya vikundi vya waasi wa ADF, FDLR na Mayi-Mayi kwenye maeneo ya Kivu Kaskazini, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC yanaupa wasiwasi Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO, wakati ambapo mamia ya raia wamekimbia makwao na kutafuta hifadhi kwenye kambi ya MONUSCO.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Kinshasa, msemaji wa vikosi vya MONUSCO, Luteni kanali Amouzoun Codjo Martin, ameeleza kwamba tarehe 29 Februari, raia 14 wameuawa na wengine 6 kujeruhiwa na ADF kwenye maeneo ya Beni,  huku askari wa jeshi la kitaifa la FARDC wakishambuliwa kwenye maeneo kadhaa.

Ameongeza kwamba kikosi cha walinda amani wa Tanzania kimepelekwa kwenye maeneo hayo ili kusaidia askari wa FARDC.

Aidha ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa mivutano ya kikabila kwenye eneo hilo baina ya jamii za waNandé na waHutu, huku waasi wa UDPI na FDLR wakishukiwa kuchochea mivutano hiyo.

(Sauti ya Luteni Kanali Amouzoun)

"Matukio hayo yamesababisha asilimia 80% ya wakazi wa kijiji cha Nyanzale kutafuta hifadhi kwenye kambi ya MONUSCO. Ujumbe wa MONUSCO kwa kushirikiana na FARDC umeongeza idadi ya walinda amani kwenye eneo hilo ili kuzuia mivutano ya kikabila na kulinda raia."