Skip to main content

Baraza la Usalama laiwekea DPRK vikwazo vikali zaidi katika historia yake

Baraza la Usalama laiwekea DPRK vikwazo vikali zaidi katika historia yake

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, limepitisha kwa kauli moja azimio namba 2270 (2016) linalolaani vikali jaribio la nyuklia lililofanywa na Jamhuri ya Watu wa Korea, DPRK (Korea Kaskazini) mnamo Januari Sita mwaka huu, na kuiwekea vikwazo vikali zaidi katika historia yake.

Aidha, Baraza hilo limekariri uamuzi wake kuwa DPRK haitofanya majaribio mengine ya nyuklia au makombora yanayotumia teknolojia ya ulipuaji, na kukomesha mpango wake wa kuunda silaha za nyuklia.

Rasimu ya azimio hilo iliandaliwa na Marekani. Akizungumza baada ya kura ya kupitisha azimio hilo, Mwakilishi wa Kudumu wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Samantha Power, amesema

Bila shaka mpango majinuni wa DPRK wa silaha za maangamizi ya halaiki, hausababishi tu mateso makubwa kwa watu wa Korea Kaskazini, lakini pia unaweka tishio la ajabu na linalozidi kukua dhidi ya amani na usalama katika rasi ya Korea, kanda, na dunia nzima. Kwa kila jaribio linalofanywa kutumia teknolojia ya ulipuaji, DPRK inaboresha uwezo wake kufanya shambulio la bomu la nyuklia, siyo tu kwa ukanda, bali pia mabara mengine. Inamaanisha uwezo wa kushambulia nyingi ya nchi zinazokaa kwenye Baraza hili. Ebu tafakari hilo.”

Kwa mujibu wa azimio hilo, kwa mara ya kwanza katika historia, shehena zote zinazoingizwa na kutoka DPRK zitafanyiwa upekuzi wa lazima. Kwa mara ya kwanza, silaha ndogondogo na silaha nyingine hazitoruhusiwa kuuzwa DPRK. Aidha, azimio hilo limeweka vikwazo vya kifedha vinavyolenga benki za DPRK na mali, na kupiga marufuku vifaa vyote vinavyohusika na nyuklia na makombora.

Aidha, vikwazo vya kisekta, na vile vinavyozuia au vinavyopiga marufuku uuzaji nje wa madini kama makaa ya mawe, chuma, dhahabu, na kupiga marufuku uuzaji wa mafuta ya usafiri wa angani na mafuta ya roketi. Vikwazo hivi pia vinalenga kukwamisha ndege za DPRK zinazoshukiwa kubeba bidhaa haramu.

Vikwazo hivyo vilivyowekewa DPRK leo ndivyo vikali zaidi kuwahi kuwekwa na Baraza la Usalama katika kipindi cha miongo miwili.