Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Shambulio jingine kaskazini mwa Mali lamulika ukosefu wa usalama

Shambulio jingine kaskazini mwa Mali lamulika ukosefu wa usalama

Nchini Mali, hali ya usalama inazidi kuzorota kaskazini mwa nchi hiyo wakati huu ambapo imeripotiwa pia mashambulizi yaliyosababisha vifo vya walinda amani sita. Inaelezwa kuwa gari la walinda amani hao lililipuka baada ya kukanyaga bomu lililokuwa limetegwa ardhini ambapo mtalaam wa Umoja wa Mataifa ameonya kuhusu kuzidi kuzorota kwa usalama. Taarifa zaidi na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora)

Taarifa ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa, MINUSMA, imesema mashambulizi ya aina hiyo ya Jumanne, hutokea karibu kila siku kwenye maeneo ya kaskazini mwa nchi.

Mtangazaji wa Redio ya Umoja wa MAtaifa nchini humo Mikado FM anaeleza zaidi Famousa Sidibe

(Sauti ya Sidibé)

"Walinda amani watatu waliojeruhiwa vibaya wamesafirishwa. Shambulio limetokea saa saba za mchana kilomita 30 kusini mwa Tessalit, kwenye maeneo ya Kidal. Vikosi vya Ujumbe wa Umoja wa Mataifa vimehakikisha usalama wa eneo hilo."

Wakati huo huo Mtalaam huru wa haki za binadamu kuhusu Mali, Suliman Baldo, ameelezea wasiwasi wake kuhusu kuendelea kwa ukwepaji sheria na ukosefu wa usalama kaskazini mwa nchi, licha ya mafanikio katika utekelezaji wa makubaliano ya amani.

Amesema hayo baada ya kutimiza ziara yake ya siku sita nchini humo, akiongeza kwamba utawala wa sheria na huduma za jamii hazijarejeshwa kwenye maeneo ya kaskazini.