Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kirusi cha Ebola chasalia kwenye maziwa ya mama, WHO yatoa mwongozo

Kirusi cha Ebola chasalia kwenye maziwa ya mama, WHO yatoa mwongozo

Shirika la afya duniani, WHO limetoa mwongozo wa muda wa uangalizi wa manusura wa ugonjwa wa Ebola baada ya kuwepo ripoti ya masalia ya virusi hivyo kwenye mbegu za kiume na maziwa ya mama.

Mwongozo huo wa muda umetolewa wakati huu kuna manusura zaidi ya 1000 wa Ebola na hivyo unalenga kupunguza madhara kwa wahanga hao na pia kuepusha maambukizi zaidi ya kirusi hicho.

Mathalani kwa upande wa maziwa ya mama, mwongozo unaeleza kuwa kirusi kimesalia kwa baadhi ya wanawake wanaonyonyesha miezi 16 tangu mama kubainika kuwa na kirusi na dalili za ugonjwa kupotea.

Kwa mantiki hiyo uchunguzi unapaswa kuendelea kubaini iwapo bado kipo au la na iwapo kipo mama anapaswa kusitisha kunyonyesha mtoto, na maziwa yaendelee kuchunguzwa kila baada ya saa 48.

WHO inapendekeza mtoto ambaye mama yake hanyonyeshi kutokana na kubainika kwa kirusi cha Ebola kwenye maziwa, apatiwe maziwa ya kopo lakini kwa kuhakikisha usafi wa hali ya juu kwa vyombo vinavyotumika ili kuepusha magonjwa.

WHO inasema inaendelea na uchunguzi kubaini muda ambao kirusi kinaendelea kuwepo mwilini hata baada ya mgonjwa kupona Ebola.