Japan imechangia dola milioni 16 wakimbizi Afghanistan na Pakistan

Japan imechangia dola milioni 16 wakimbizi Afghanistan na Pakistan

Serikali ya Japan Jumatano imetangaza mchango wa dola milioni 16 kwa mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa likiwemo la mpango wa maendeleo UNDP, la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la kuhudumia watoto UNICEF na la mpango wa chakula WFP ili kusaidia watu wanaorejea katika maeneo ya kikabila FATA na wakimbizi wa Afghanistan nchini Pakistan.

Afisa wa ubalozi wa Japan nchini Pakistan Bwana Junya Matsuura na mratibu mkazi wa Umoja wa Mataifa  bwana Neil Buhne wametangaza kuhusu msaada huo kwenye ofisi za WFP mjini Islamabaad.

Dola hizo milioni 16 zitaganywa kwa mashirika hayo ambapo milioni 3 zitakwenda kwa UNDP, milioni 4 kwa UNHCR, milioni 3 kwa UNICEF na milioni 6 kwa WFP kutumika kwa ajili ya miradi mbalimbali.

Miradi hiyo ni pamoja na kuwezesha utawala wa kikabila na kuwasaidia wanaorejea katika maeneo hayo ya FATA, pia kutoa msaada wa ulinzi elimu, mafunzo ya ufundi stadi kwa wakimbizi vijana wa Afghanistan wanaorejea nyumbani.

UNICEF itatumia fedha hizo kwa kujikita kwa afya ya mama na mto katika maeneo ya FATA,ikiwemo kuwapa maji safi, huku WFP ikihakikisha wanaorejea wanapata lishe bora. Mwaka 2015 Japan ilitoa tena mchango wa dola milioni 18.4 kuwasaidia wanaorejea na wakimbizi wa Afghanistan walioko Pakistan.