Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wanaoteseka zaidi wamulikwa na Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa

Wanaoteseka zaidi wamulikwa na Benki ya Dunia na Umoja wa Mataifa

Hapatakuwa na maendeleo wala amani, bila kuheshimu haki za binadamu, amekariri leo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Jan Eliasson, akihutubia mkutano wa Benki ya Dunia uliofanyika leo mjini Washington, Marekani kuhusu udhaifu, mizozo na ukatili.

Lengo la mkutano huo ni kuzungumzia jinsi ya kukuza jamii jumuishi zaidi ili kupunguza tofauti za kiuchumi na kuendeleza amani.

Bwana Eliasson ameelezea mapendekezo matatu anayotaka kuyawekea kipaumbele.

Amesema la kwanza ni umuhimu wa kuzuia mizozo, ikiwa kupitia ufadhili wa muda mrefu ili kukuza utulivu wa nchi.

Ametaja la pili kuwa ni kupunguza mahitaji ya kibinadamu, akiongeza kwamba mahitaji yanazidi uwezo wa jamii ya kimataifa wa kuyafadhili.

Hatimaye amemulika umuhimu wa kukuza amani endelevu kwa kuhudumia wanaoteseka zaidi kwenye jamii na kuendeleza uwezo wa nchi husika kupitia ushirikiano wa kimataifa.

Kwa mujibu wa Benki ya Dunia, zaidi ya watu 600 na wadau 100 wamehudhuria mkutano huo.