Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Tutasusia vikao vinavyojadili haki za binadamu DPRK, aonya Waziri Ri

Tutasusia vikao vinavyojadili haki za binadamu DPRK, aonya Waziri Ri

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea imesema kuwa haitoshiriki vikao vya kimataifa vinavyomulika hali ya haki za binadamu katika DPRK kwa minajili ya hujuma za kisiasa tu.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi, wakati wa kikao cha 31 cha Baraza la Haki za Binadamu, Waziri wa Mambo ya Nje wa DPRK, Ri Su-Young, amesema hujuma hizo za kisiasa ni kinyume na maazimio kadhaa ya Umoja wa Mataifa na vuguvugu la nchi zisizofungamana na upande wowote, ambayo yanapinga vikao kugeuzwa kuwa vya kisiasa, na kutaka hujuma za kisiasa zikomeshwe katika kushughulikia masuala ya haki za binadamu za nchi binafsi.

Amesema maazimio yoyote yatakayopitishwa dhidi ya DPRK katika vikao kama hivyo, yataendelea kuwa ushahidi wa upendeleo na unafiki.

Balozi Ri ameongeza kuwa hata maazimio kama hayo yakipigiwa kura au yasipigiwe kura, hawatojali, na kamwe hawatayaheshimu.

Amesema inasikitisha kuwa hali katika Baraza la Haki za Binadamu inazidi kuzorota, akihitimisha kuwa inatia aibu kwamba Baraza la Haki za Binadamu limegeuzwa kuwa mfumo kamili wa kisiasa.