Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF, WHO na serikali ya Syria zakubaliana kuhusu chanjo kwa watoto

UNICEF, WHO na serikali ya Syria zakubaliana kuhusu chanjo kwa watoto

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Anthony Lake, amesema kuwa serikali ya Syria imekubali kushirikiana na Shirika la Afya Duniani, WHO na wadau wengine katika kuandaa na kutekeleza mpango wa kitaifa wa utoaji chanjo dhidi ya magonjwa yanayowaathiri watoto.

Hata hivyo, Bwana Lake amesema utekelezaji wa mpango huo utahitaji pande kinzani ziwezeshe ufikiaji wa maeneo yaliyozingirwa na yenye ugumu kufikiwa, na kwamba serikali na vikundi kinzani vyenye silaha vitawezesha ufikiaji wa watoto wote wa Syria.

Mkurugenzi huyo wa UNICEF amesema hayo baada ya ziara yake nchini Syria, ambako ametembelea miji ya Damascus, Homs, Hama na Al-Salameya, na kusikia watu wakizungumzia matumaini yao kwamba kutakuwa na amani inayozidi maandishi kwenye karatasi za kidiplomasia ili waweze kuishi maisha ya amani.

Kufikia kesho Jumatano Machi Mosi, mzozo wa Syria utakuwa umedumu kwa muda wa miaka mitano, ukiwa umesababisha uharibifu mkubwa na taabu kubwa kwa watoto.