Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baraza la Usalama kujadili azimio la vikwazo vikali dhidi ya DPRK

Baraza la Usalama kujadili azimio la vikwazo vikali dhidi ya DPRK

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, linatarajiwa kukutana kesho Jumatano, kujadili rasimu ya azimio kuhusu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, DPRK, likitarajia kuiwekea nchi hiyo vikwazo vipya na kuiwekea shinikizo zaidi, kufuatia jaribio lake la zana za nyuklia mnamo Januari Sita mwaka huu.

Awali, akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Mwakilishi wa Marekani kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Samantha Power, amesema azimio hilo lililoandaliwa na Marekani, lilijadiliwa kwanza kati ya Marekani na Uchina kabla ya kuwasilishwa kwa wajumbe wa Baraza la Usalama wakati wa mashauriano yao mnamo Februari 25 2016.

Iwapo litapitishwa, azimio hilo ambalo limechukuwa muda mrefu zaidi kujadiliwa ikilinganishwa na maazimio ya awali, litaweka duru ya tano ya vikwazo dhidi ya DPRK tangu mwaka 2006, ambavyo Balozi Power ametaja kuwa vyenye nguvu zaidi kuwahi kuwekwa na Baraza la Usalama katika kipindi cha miongo miwili.

Hapa, Balozi Samantha Power anataja baadhi ya vikwazo hivyo

Kwa mara ya kwanza katika historia, shehena zote zinazoingizwa na kutoka DPRK zitafanyiwa upekuzi wa lazima. Kwa mara ya kwanza, silaha ndogondogo na silaha nyingine hazitoruhusiwa kuuzwa DPRK. Aidha, azimio hili litaweka vikwazo vya kifedha vinavyolenga benki za DPRK na mali, na kupiga marufuku vifaa vyote vinavyohusika na nyuklia na makombora.”

Aidha, kwa mara ya kwanza, Balozi Samantha Power amesema azimio hilo litaweka vikwazo vya kisekta, na vile vinavyozuia au vinavyopiga marufuku uuzaji nje wa madini kama makaa ya mawe, chuma, dhahabu, na akaenda mbali zaidi

Na kupiga marufuku uuzaji wa mafuta ya usafiri wa angani na mafuta ya roketi. Vikwazo hivi pia vitakwamisha ndege za DPRK zinazoshukiwa kubeba bidhaa haramu”