Canada yawapatia hifadhi wakimbizi 25,000

Canada yawapatia hifadhi wakimbizi 25,000

Canada imetimiza ahadi yake ya kupokea wakimbizi wa Syria 25,000, limesema leo Shirika la Kimataifa la Uhamiaji IOM.

Kwenye taarifa yake IOM imesema Canada ilitoa ahadi hiyo mwisho wa mwaka 2015 na jumatatu hii ilikuwa ni safari ya mwisho ya wakimbizi kutoka Jordan, Uturuki na Lebanon.

IOM imesema wakimbizi hao 25,000 wamesafirishwa kwa kipindi cha miezi mitatu tu, huku kawaida shirika hilo likisaidia wakimbizi wapatao 30,000 kila mwaka kupata makazi mapya duniani kote.

Mpango wa dharura wa kupeleka idadi hiyo kubwa umeandaliwa na IOM kwa ushirikiano na Shirika la Umoja wa MAtaifa la Kuhudumia Wakimbizi UNHCR, serikali za nchi husika na wadau wengine.