Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi, heshima kwa wote ni msingi-Ban

Siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi, heshima kwa wote ni msingi-Ban

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya kupinga ubaguzi, jumuiya ya kimataifa imetakiwa kukubali utofauti uliopo kati ya makundi ya watu, kuheshimu na kusaidiana ikiwa ni hatua muhimu katika kutokomeza vitendo vya kibaguzi. Grace Kaneiya na taarifa zaidi.

(TAARIFA YA GRACE)

Kauli mbiu ya mwaka huu ni jitokeze, hamasisha kila mmoja kutetea jamii ya haki ambapo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema pale ambapo jamii za pembezoni na hatarishi zinapobaguliwa , watu wote hudidimia  na akasema kuwa Umoja huo umejizatiti kuinua haki za binadamu na utu kwa wote.

Siku hii adhimu huangazia ubaguzi katika nyanja tofauti ambapo shirika la Umoja wa Mataifa la makabilianao dhidi ya Ukimwi UNAIDS katika taarifa yake linasema kuwa ubaguzi umeenea zaidi katika misingi ya kjinsia, kitaifa, umri, makabila, asili na hata katika misingi ya dini.

Takwimu zinaonyesha kuwa nchi nne kati ya kumi duniani ndizo zina mgawanyo sawa wa mahudhurio ya wavulana na wasichana katika shule za sekondari huku pia ubaguzi katika sekta ya afya ukitajwa kuenea zaidi.

Katika ujumbe wake kwa njia ya video Mkurugenzi Mtendaji wa UNAIDS Michel Sidibé anasema.

(SAUTI MICHEL)

‘Watu hawapati huduma kwasababu ya mwelekeo wao wa kimapenzi ,tunaogopa kwa kuwa uzoefu unatuonyesha kuwa ikiwa una virusi vya ukimwi ukitengwa unaangamia. Ubaguzi ulikuwa ni moja ya vipingamizi vikubwa katika vita dhidi ya Ebola. Kwa hakika tunahitaji kuhamasishana.’’