Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mjumbe wa amani wa UM Leonardo DiCaprio ashinda tuzo ya Oscar

Mjumbe wa amani wa UM Leonardo DiCaprio ashinda tuzo ya Oscar

Mcheza filamu nyota wa Marekani na mjumbe wa amani wa Umoja wa Mataifa Leonardo DiCaprio ni miongoni mwa washindi wakubwa katika tuzo za Academy mjini Hollywood zilizotolewa Jumapili usiku.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 ambaye labda anajulikana sana kwa kushiriki filamu ya  'Titanic, amejishindia Oscar ya kuwa mwigizaji bora kutokana na ushiriki wake katika filamu ya 'The Revenant.'

Bwana DiCaprio aliteuliwa kuwa mjumbe wa Amani wa Umoja wa Mataifa kwa mtazamo maalumu unaolenga mabadiliko ya tabianchi  mnamo mwaka 2014. Alitumia fursa ya kutoa hotuba yake ya ushindi kutanabaisha kuhusu suala la mabadiliko ya tabianchi, akisema ni suala ambalo lipo bayana na linatokea sasa.

Bwana DiCaprio alikuwa miongoni mwa watu mashuhuri waliohudhuria mkutano wa Umoja wa mataifa wa mabadiliko ya tabianchi uliofanyika Paris Disemba mwaka jana.